CONSTITUTIONA WRITING

Sunday, January 19, 2014

ELIMU NA HATIMA YA TANZANIA

         Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo mfumo wa elimu umeshindwa kuleta mabadiliko ya kweli ya kujenga taifa linalojitegemea. Tusipokuwa makini itakuwa vigumu kujenga taifa la watu wanaojitambua na hatimaye kuendelea kuwa na kizazi cha watumwa wa ukoloni mambo leo. Sishangai kwa hatua ya serikali kuruhusu walioshindwa kufikisha viwango vya ufaulu mtihani wa kidato cha pili 2013, kuruhusiwa kuendelea na masomo ya kidato cha nne. Haya yote yanatokea kutokana na kutokuwa na falsafa madhubuti inayoongoza wizara ya elimu kama itikadi ya nchi. Mara nyingi mtizamo wa maendeleo ya elimu hapa nchini kwetu imekuwa ni kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wanaohudhuria kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu huku kipimo cha elimu kikiwa ni ufaulu wa vyeti.
     Miongozo mbalimbali ikiwemo MKUKUTA  sura ya tatu inazungumzia  maisha bora na ustawi wa jamii lengo namba tatu linaelezwa kuwa ni upatikanaji wa elimu bora ya msingi na sekondari kwa wasichana na wavulana, elimu ya watu wazima kwa wote miongoni mwa wanawake na wanaume na upanuzi wa elimu ya juu na elimu ya ufundi. Dhana hii imejengwa katika kuongeza idadi na suala la ubora  na wanafunzi wa sampuli gani halijapewa kipaumbele. Kwa mfano taarifa ya utekelezaji wa MKUKUTA 2009/2010 iliyotolewa na wizara ya fedha na uchumi inasema kuwa kumekuwepo ongezeko kuhusu maendeleo ya elimu kwa kutaja takwimu ambazo kimsingi ni vigumu kupima ubora wake na mchango wa maendeleo ya ongezeko hilo kwa  taifa na jamii kwa ujumla. 
   Taarifa hii na nyingine nyingi zitolewazo kwa kufata mwongozo wa MKUKUTA kwa mtizamo wangu naona siyo sahii kupima ubora wa maendeleo ya elimu Tanzania bali mchango wa wanafunzi wanaohitimu uwe ndio kipimo cha maendeleo hapa nchini. Kipimo cha ubora kiende sambamba na jinsi ongezeko la wahitimu na kupungua kwa matatizo mbalimbali ya kijamii. Fikra ile ile ya kuangalia takwimu imejipenyeza hata kwenye Mpango wa matokeo makubwa sasa (Big Results Now) ambao kwa upande wa elimu, Halmashauri zimepewa jukumu la kutumia rasilimali chache walionazo kuhakikisha ufaulu unaongezeka. Wakati haya yakiendelea wanazuoni mbalimbali wamekuwa wakihoji kuhusu mitaala inayofundishwa Tanzania kuwa inawajenga wanafunzi kukariri na sikuwa wadadisi na wagunduzi wa mambo mbalimbali yenye kuleta tija kwa taifa letu.
    Tanzania imeruhusu watu wanaopewa nguvu ya kuongoza wizara kila mtu kuja na mpango wake ambao unakuwa na maneno tofauti lakini ukichambua kwa kina mfiumo inayoweza kuleta fikra mpya kwa wanafunzi haibadiliki. Kibaya zaidi ni enzi za  Mheshimiwa Joseph Mungai aliyefuta masomo ya kilimo kwa shule za sekondari na wakati inajulikana kabisa asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini na uchumi wao mkubwa unaotegemewa ni  kilimo. Tangu mvurugano huu kujitokeza nchi imekuwa ikirudi nyuma kila kukicha. Si sera wala viongozi wapya wanaopewa dhamana wanabadili kitu isipokuwa kufanya marekebisho yakushusha viwango vya ufaulu ilimradi wanafunzi wengi waendelee na ngazi za juu zaidi huku wakiwa hawakidhi vigezo.
   Elimu imefwanywa bidhaa kama unavyoweza kununua sokoni huku ikijenga makundi miongoni mwa watanzania. Wale wenye kuaminika kuwa na ukwasi mwingi wao wanajitenga na watoto wa masikini kwa kusoma shule maalum zinazolipiwa ghrama kubwa. Watoto wa maskini wameundiwa shule maalum za kata ambazo nimara chache kukuta watoto wa viongozi wakubwa kama mawaziri , viongozi na matajiri. Pamoja na mgawanyiko huo hamanishi kwamba wanaokwenda shule za binafsi wanapata elimu bora kwani wanajengwa katika mazingira yakuweza kufaului kupata vyeti vizuri vya kuwawezesha kuingia soko la utumwa wa karne ya 21 ambayo ni kuajiriwa. Mwalimu Nyerere kwenye miaka ya 1964 alianzisha falsafa ya elimu ambayo ililenga taifa linalojitegemea kwa kusisitiza elimu ya kujitegemea. Kuwajengea uwezo wa Tanzania kuweza kuvuna rasilimali zao wenyewe kuliko ilivyo sasa Tanzania haina wataalamu wakuvuna rasilimali zetu kama gesi, madini na nyingine zinazoendelea kugunduliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Tumeshindwa kuwajenga Watanzania kuwa na uwezo wa technolojia ambayo imepelekea rasilimali muhimu kukabidhiwa kwa makampuni mengi ya kigeni ambayo yanachukua faida kubwa itokanayo na rasilimali zetu kuliko kama tungetumia wataalamu wetu -waiosomeshwa kwa kodi zetu. Hata tunaowaita wataalam wamekuwa watumwa wa utaalam wao.
           Tumekimbizana na utandawazi wa kuruhusu wawekezaji wa nje kwa misingi kwamba dunia imekuwa kijiji kimoja. Lakini kwa kufanya hivyo tumeshindwa kuwa na majibu kuwa ni Watanzania wangapi wanauwezo wa kuwekeza katika mataifa makubwa , wanawekeza katika nini na taifa linanufaikaje.Kwa kufanya hivyo soko tumeliacha lijiendeshe bila kuangalia nafasi yetui  katika utandawazi. Mwaka 1998 wakati Mwalimu Nyerere anatunukiwa shahada ya heshima kutoka     chuo kikuu huria cha Tanzania alisema "....... as we prepare ourselves for a competitive life in the Global village, we must not forget  that our corner stone  is going to be in rural Tanzania or the informal sector of urban Tanzania.
     Watunga sera tulionao wamekuwa watu wakukopi na kupesti  pamoja kupokea mshinikizo ya wafadhili kutoka nchi  za magharibi bila kuangalia uwezekano wa kutekeleza mifumo ya kimagharibi katika jamii ya Kitanzania. Watu wanafikiri kama vile vijiji vya Tanzania hawavijui. Lakini kwa hili si shangai linatokana na watu kupewa vitengo ambavyo hawana weledi navyo. Hauwezi ukawa na mchumi peke yake au mtu aliyebobea kwenye mitaala ya elimu bila kumhusisha msosholojia ambaye amebobea katika uchambuzi wa sera za kijamii na mchango unaotolewa na sera husika katika kuboresha maisha ya watu. Kwa uchambuzi wa kisosholojia unaenda mbali zaidi kutathmini utofauti wa aliye hitimu la saba na yule ambaye hajafika kabisa, tofauti kati ya kidato cha nne na darasa la saba na aliyehitimu chuo kikuu na aliyehitimu stashahada. Tusipoweza kung'amua ubora na michango ya watu hawa hata kama udahili utaongezeka mara mia huku hauendani    na majibu ya changamoto zinazoikumba jamii ni viogumu kusema kuwa elimu imeboreshwa Tanzania.
         Mao Tse Tung katika kitabu chake  1966 (selected speeches ) anatufundisha umuhimu wakujifunza kutokana na makosa. Hivyo kukosea kwa binadamu kupo tukubali tuna paala tulikosea ndio maana tumeendelea kuwa na utegemezi wa teknolojia katika uvunaji rasilimali zetu na kuendelea kuzalisha wasomi ambao ni watumwa wa kuajiriwa na kushadadia wazungu.
TUFANYE  NINI?
          Kutokana na ukweli kwamba elimu hii imekuwa ikipigiwa kelele marakwa mara bila majibu na kwa kuwa watu wengi wamesoma lakini bado wameendelea kuwa watumwa wa elimu zao sambamba na nchi kuendelea kutegemea wataalam na makampuni ya nje nashauri mambo yafuatayo kufanyika ili kuleta mabadiliko ya kweli na kujega taifa imara linalojitosheleza kifkra na kiteknolojia mambo yafuatayo yafanyike.
       Kuwepo na mtizamo na falsafa mpya yakuongoza wizara ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu. Tunahitaji falsafa ambayo itapandikiza chachu ya wasomi kujitegemea na kuja na mabo mapya. Kwamfano kama sasa mtu anasoma ili kuajiriwe kwenye taasisi kubwa basi mwanafunzi aanze kusoma akiwa na fikra ya kutengeneza fursa yakuajiri na kulipa mishaara mikubwa. Pia mwanafunzi ajengwe kutodharau kazi na kutoingiliwa na wanasiasa katika harakati za kujitafutia maisha ilimradi havunji sheria.

     
Pili kama taifa tuwe na vibaumbele katika elimu inayotolewa huku misingi mikuu ikiwa ni kuwa na wataalamu wa uzalishaji katika kilimo waliojiari wenyewe na serikali itoe fursa na maeneo maalumu kwa vijana watakaohitimu wakataka kujikita katika kilimo. Kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa na kinaweza kuajiri watu wengi. Hivyo katika mabadiliko ya falsafa na dhana ya elimu, somo la kilimo liwe la lazima kuanzia darasa la awali huku likihuisha na mazingira yetu. Wataalam wa saikolojia wanasema mwanafunzi ukimfundisha katika mambo yanayoendana na mazingira pamoja na vitendo  anaelewa haraka na kuthamini ujuzi anao pewa. Kwa hili kuna baadhi ya shule nimejifunza kwa mfano shule ya Sekondari Weruweru  katika maadhimisho ya miaka  50, wameonyesha kitu cha utofauti wanafunzi wana muda wa kwenda shamba na shamba kweli ukiliona linaonyesha lipo kwenye taasisi ya elimu kutokana na ubora wake. Siyo hilo tu bali ata utashi kwa wanafunzi ni mkubwa kujisomea na kufanya kazi. Kama  taarifa zilizokuwa zinarushwa na kituo cha    chaneli ten ni za kweli basi kama wizara ina haja yakushirikisha uzoefu wa shule hii katika kuimarisha sera na miongozo ya elimu Tanzania.
      Tukiachana na kilimo pia tunahaja yakufanya tathmini ni wapi tunapwaya kiteknolojia ili tuweze kuwaandaa vijana wa Kitanzania kusoma fani ambazo zina umuhimu katika kuvuna rasilimali za nchi yetu. Tuitafute teknolojia popote pale duniani hasa katika mambo ya gesi, mafuta, madini na teknolojia ya umwagiliaji ili tusiwe wasindiokizaji katika utandawazi. Kama viongozi wanaweza kusafiri nje kwa safari zisizo na tija iweje ishindikane kila mwaka kupeleka vijana wakitanzania zaidi ya 50 kila mwaka kuisaka teknolojia. Ili kuhakikisha tunaondokana na kukimbiwa na wataalam tuliowasomesha (brain drain), tuwasainishe mikataba ambayo itawafanya kurudi nyumbani baada ya masomo.  Sambamba na hilo tuwe na makampuni ya serikali yaliyojikita kwa kila sekta kama gesi, mafuta nk. ili ikitokea nchi anawahitaji wataalam wetu serikali iwe inalipya kwa kuwatumia wataalam  watakaosomeshwa na kodi za Watanzania (consultancy services).
         Tukisha kuwa na hawa wataalamu tuwape kinga wasiingiliwe na wanasiasa maana ndio chanzo cha kushusha morali na uzalendo kwa wataalam. Hata asiyekuwa na ABC kwenye kitu fulani anajifanya kuwa anajua kila kitu na kuzalilisha taaluma za watu wengine. Tukiwawezesha vijana kusoma fani ambazo zina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi ni sehemu moja wapo ya kutoa hamasa kwa vijana wengi wa Kitanzania kupenda masomo ya sayansi. Ili kufanikisha hili, kwa kuanza serikali inatatakiwa kuwa na na shule maalum kuanzia msingi zitakazojengwa katika itikadi na mchepuo wa ujuzi fulani ili hatimaye wakiendelea na masomo ya juu zaidi wawe na msingi imara na isiwe kusubiri mtu amalize kidato cha sita alafu aende kwenye fani fulani. Nimetumia neno serikali makusudi tusiiachie sekta binafsi maana sekta binafsi inalenga kwenye faida na inaweza kutoa mwanya kwa wenye pesa pekee kuwa ndio wanufaika wakuu wa programu hii. Kwangu mimi sioni kama haiwekani kama tukiwa na utashi wa kisiasa, uzalendo na utaifa badala yakujikita katika vyama vya siasa vinavyopambana kutawala dola na si taifa linalojitegemea.
        Tatu kufanya mabadiliko katika upatikanaji wa wataalam wa sera na utafiti kuhusu mambo ya elimu. Lazima kuwepo na wasosholojia na wataalam wengine hasa walijikita katika mambo ya elimu. Tukiwa na watunga sera kutoka fani moja ya elimu au wachumi bila wasosholojia bado kupata falsafa na dhana ya elimu tuitakayo itakuwa ndoto.
         Nne mfumo wa ufundishaji uwe wa vitendo zaidi kuliko nadhalia ili wanafunzi kujengewa uwezo wa kuweza kutumia uzoefu kubuni vitu  vipya na vyenye tija kwenye jamii kuliko   ilivyosasa ambapo mwanafunzi anakesha akisoma ilikufikisha viwango vya ufaulu vilivyowekwa huku akiwa na fikra mgando katika kung'amua mambo. Msomi cheti kwa sasa hana nafasi kwa kipindi ilikuwa enzi hizo.Tubadilike ilikuendana na kasi ya utandawazi na kujinasua na ukoloni mambo leo ambao tusipokuwa makini utaimaliza Tanzania na Afrika kwa ujumla.
     Tano tuache tabia za kubebana kukabidhi majukumu makubwa kwa watu amabo hawana maono wala utashi-watu ambao wanalewa madaraka . Kuna watu wanapopewa vitengo anajiona kana kwamba yeye ni Tanzania one katika hiyo fani kumbe wengine ni kwasababu tu yakuwa karibu na watawala na kama kumngekuwepo na uwanja wa wazi kushindania nafasi hiyoasingeweza kutamba. Kupewa na fasi bado unafursa kutumia mawazo ya wanaofikria zaidi yako kufanya mabadiliko. Wengine, wakishapata, hudharau waliochini yao suala ambalo siyo sahii. Elimu siyo mchezo wa timu moja bali nishirikishi-tunahitaji kuchanganya mawazo, kupingana kwa hoja na hatimaye kujenga muafaka na hatimaye kuwa na mtizamo mmoja kama nchi. 
        Mwisho nchi ni yetu sote matunda mabaya ya mfumo wa elimu yanamathiri kila mtu hivyo tuungane kuboresha. Lakini katika kuboresha siasa zetu chafu tuweke pembeni tuwe na mwafaka wa nchi na falsafa moja. Hii itatusaidia kuzuia waziri mpya au chama kipya kitakochoingia madarakani kuvuruga elimu yetu na hatimaye kuwa na mfumo bora ambao unazalisha wasomi wenye tija katika taifa.Tangia sasa kubebana iwe mwiko kwa kila mtu. Tukisha kuwa na mmwafaka katika elimu basi naamini ata shule zetu, mfumo wakupata walimu na mazingira yakujisomea yataboreshwa. Lakini tukiendelea elimu kuifanya agenda yakisiasa tunachezea uchumi wa nchi yetu na kuroga maendeleo yetu wenyewe. Maisha tunaishi kwa sasa yaelimu isiyo  na tija baada ya miaka kumi iwe ni historia kwani tukifanya haya mabadiliko yatapatikana.
HAYO NI MAWAZO YANGU. NAOMBA KUWASILISHA.NA HAYAWAKILISHI TAASISI AU MWAJIRI WANGU.
Godfrey Vedasto
Mshauri na mchambuzi wa sera za kijamii
07121357/0789915677
       

Wednesday, January 1, 2014

WATU HATARI

                  Kuna watu wa ajabu wenye mambo ya kushangaza katika dunia hii. Kutokana na imani yangu Mungu tunaye mmoja na ndiye anayestaili kuabudiwa. Lakini wanadamu baadhi wamejifanya kuwa miungu watu  kutokana na sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza msingi wake unatokana na kuwa na mamlaka juu ya  watu wengine. Mamlaka yamewanya baadhi ya watu wawadharau wengine hadi  kuwadhalilisha utu wao. Sababu ya pili ni kuwa na umiliki wa mali (rasilimali pesa). Kuna baadhi ya watu wanataka kuabudiwa na kujiona kwamba kila wanachosema ni sahihi kuliko wengine. Sababu nyingine ambayo kwa sasa haina nguvu sana ni elimu. Kwamaana unaweza ukawa na elimu lakini kama hauna mamlaka ya kiutawala au pesa au kuwa karibu na watawala unaweza usiwe na nguvu katika dunia ya sasa. Lakini pamoja na hayo kuna watu wanotumia mwanya wa ujinga wa watu kuwatawa kifikra hali ambayo utengeneza umungu MTU.
            Hali hii yakutaka kuabudiwa imekuwa ndiyo chanzo cha migogoro mbalimbali inayoendelea hapa duniani. Ukichambua kwa kina  utaona  hawa watu wanaojiona bora zaidi ya wengine ni wale ambao hofu ya Mungu haipo ndani ya mioyo yao. Makundi haya yamwshika   hatamu si kwenye siasa bali hata kwenye majumba ya ibada kama makanisa na misikiti. Ndiyo wanaopewa kipaumbele kwa mambo mengi.

      Pia watu wanojiona bora zaidi ya wenzao huwa na sifa ya ubinafssi. Ukimkuta ofisini mali ya umma anaitumia kama vile ni mali yake. Mtu wa  sampuli hii ni mwepesi kuchukua hatua kali kwa waliochini yake pindi wanapokosea huku akisahau maovu ambayo anayafanya yeye    mwenyewe.  Akiachishwa cheo huwa siyo wepesi wakuonyesha ushirikiano bali huwa na majungu na ni hatari kwani wanaweza kufanya mbinu zozote zile mbaya amabzo zinaweza kumhatarisha mtu mwingine aliyepewa hiyo nafasi.
     Mara nyingi hawa watu wakujikweza na kupenda kuabudiwa, huwa ni wanafiki ikiwa na maana kwamba hupenda kuonekana wasafi mbele za watu kwa gharama zozote iwe kwa kutumia cheo au pesa ili mradi jamii iwaone wanafaa. Watu hawa, vigumu kuleta mabadiliko kani  wao wenyewe hawajabadilika (not transformed therefore it is difficult to transform others).
     Kutokana na tabia za watu hawa husababisha migogoro kujitokeza kati yao na jamii. Kwa mfano mwenye mamlaka akiwadharau waliochini yake hawatamheshimu na matokeo yake kama ni wafanya kazi utafuta sababu na mbinu za kumwonyesha kwamba hawamkubali. Kwa kufanya hivyo migogoro upamba moto.
    Kwa mwenye pesa utaka kumiliki kila nyenzo muhimu katika maisha ikiwa ni pamoja kupanga bei sokoni na kudhulumu rasilimali za wanyonge. Na wanyonge wakijitambua wakaona wanafanyiwa ndivyo sivyo upambana kwa migomo na maandamano kwa maana sheria mara nyingi huwa upande wa mwenye pesa na hata akiwa na kosa mamlaka zinazohusika umwajibisha kifallme suala amabalo huchochea migogoro kwa wananchi.
         Ukikosa hofu ya Mungu kama binadamu inapelekea mtu kutokuwa na hekima na busara matokeo yake ni kutoa maamuzi kwa misingi yakutaka kujiona bora zaidi na kudharau wengine kwa misingi ya fedha, elimu na nafasi/ mamlaka aliyonayo mtu. Pia hali hii huchochea kutotendeka kwa haki na ibinadamu hatimaye migogoro. Wanadamu wamekengeuka mpaka kufikia hatua ya kuwajeruhi watu wengine kimwili na kiroho ambao harakati zao zinapingaukiukwaji wa haki za binadamu na unyonyaji.