CONSTITUTIONA WRITING

Monday, September 30, 2013

WAZEE WETU TUWAENZI

   Ndugu wapendwa katika Bwana  , tarehe 1/10/2013 ni maadhimisho  ya siku wazee. Kwa hapa nchini kwetu yanafanyikia Korogwe mkoani Tanga. Katika madhimisho hayo wazee kutoka mikoa mbalimbali wataungana  kusherehekea siku hii ya muhimu sana. Natoa wito kwa Watanzania kuwaunga mkono kwa kufanya mambo yenye utofauti ambayo kwayo upendo unaweza kujidhihirisha. Wazee hawa ni tunu na wana mengi ambayo sisi kama vijana tunajifunza kwao. Wazee hawa wana mchango mkubwa katika kutujenga kifikra na kimawazo kwani kuishi kwao kwingi wameona mengi na wanayo mengi tunayojifunza kutokana na uzoefu wao.
     Nashauri mambo yafuatayo katika kuwakumbuka wazee ili waweze kuona utofauti na siku zote
Kwanza tujitolee kuwasaidia wazee ambao hawana msaada kabisa walau kuwafanyia shughuli  yoyote kwa mfano kuwafulia nguo, kuwachotea maji au chochote kile ambacho unaona unaweza kukifanya.
    Pili, tuwapigie simu kwa wale ambao wako mbali . Hali hii itawafanya wafurahi na kuona kuwa jamii/ndugu wanawasamini. Pia katika maongezi yetu iwe kwa njia ya simu au uso kwa uso  yaambatane na utani waweze kuburudika na kupunguza msongo wa mawazo. Katika jamii zetu kuna  baadhi ya wazee wanaokosa watu wa kuwatania hivyo wanajisikia vibaya kama wametengwa na jamii.
      Tatu tuwaombee ili Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa nguvu za kimwili na kiroho. Tunajua wazee wetu wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali  hivyo tukiwa karibu nao kwa njia ya  dua kila mtu kwa imani yake naamini tutaweza kuimarisha mioyo yao na hatimaye kuendelea kuwa na afya njema huku wajukuu na vitukuu wakiendelea kunufaika kutokana na busara na baraka za wazee wetu.
     Nne, kwa watunga sera  na vyombo mbalimbali vya maamuzi sasa vione haja yakutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha ustawi ulio bora kwa wazee. Wazee wasitajwe kwa misingi ya kujizolea umaharufu kisiasa bali tunapowataja kweli iwepo ndani ya mioyo yetu hata matendo  yadhirishe tunayyatamka. Imezoeleka wakati wa chaguzi watu   ndo huwaona wazee wa maana wakishapata ndo basi tena. Kama tunawapangia bajeti tuhakikishe fedha za miradi ya wazee zinakuja kwa wakati.
       Tano, kama jamii ipangwe mikakati mahususi ya kuwasaidia wazee wasio na uwezo kupitia serikali zetu za vijiji au mitaa. Tusiwaache wenyewe maana kila mtu anaelekea uzeeni. Kwa kadili watoto watakavyoona wazee wanavyotunzwa na jamii tutakuwa tumetengeneza mnyororo wa uhakika wa hifadhi ya jamii kwa wazee. Kuanzia ngazi ya familia isiwe huyu ni babu mdogo au bibi mdogo wote hawa ni ndugu zetu baraka zao nikubwa katika mafaniko yetu. Inashangaza kuona watu wako mijini wanakula starehe huku babu, bibi , shangazi, mjomba hata wazazi wao wanateseka vijijini. Kunauwezekano ugumu wa maisha na kutofanikiwa  ni  laana inayotokana na kutowajali wazee.
       Mwisho nina imani tukiyazingatoia haya tutaweza kuwa na jamii inayowathaminini wazee. Lakini la muhimu zaidi tukiawajali wazee tunaweza kuongeza miaka ya kuishi kwani mtu akifika uzeeni hatakuwa na msongo wa mawazo, hatajisikia mpweke bali atakuwa na nguvu na utulivu wa akili hivyo kumpunguzia magonjwa kama ya moyo ambayo yanaweza kusababishwa na kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kutokuwa na kinga ya kijamii  endelevu na yenye uhakika kwao.

Imeandaliwa na:
Afisa Ustawi wa Jamii na mshauri wa kisaikolojia
HANDENI-TANGA
E-mail :gkanjara@gmail.com
0712135799

No comments :

Post a Comment